Sunday, December 24, 2017

WAZIRI MKUU AMTAKA AFISA ARDHI MANISPAA SONGEA KUMALIZA TATIZO LA MAMA ALIYEDHULUMIWA NYUMBA YA URITHI


Mkazi wa Msamala katika Manispaa ya Songea, Monica Joseph Miti akitoa maelezo yake mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (Hayupo pichani) kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Mwengemshindo ambapo Bibi Miti aliomba asaidiwe kurejeshewa nyumba yake aliyotapeliwa na mtumishi wa Manispaa hiyo baada ya mumewe kufariki dunia.
Na Kassian Nyandindi,        
Songea.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Afisa ardhi wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Kundaeli Fanuel Ndemfoo afuatilie suala la Bibi Monica Joseph Miti na wanae ambao walidhulumiwa nyumba ya urithi na aliyekuwa mwanasheria wa Manispaa hiyo.

Alitoa agizo hilo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kata ya Mwengemshindo baada ya kupokea bango lililoandikwa na Bibi Miti kuomba arejeshewe umiliki wa nyumba ya marehemu muwewe.

Alipopewa nafasi ya kueleza tatizo lake, Bibi Miti ambaye alimtaja mwanasheria huyo kwa jina moja la Mwakasungura, alidai kuwa mwanasheria huyo alighushi hati ya nyumba na kuwatoa ndani ya nyumba yeye na watoto wa marehemu. 


Alipoulizwa na Waziri Mkuu aeleze alipo huyo mwanasheria, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Tina Sekambo alijibu kwamba alishahamishiwa wilaya ya Ukerewe.

Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea na Afisa ardhi wa Manispaa hiyo wafuatilie suala hilo na wampe majibu mapema iwezekanavyo. 

Hata hivyo amemuomba Bibi Miti na wanawe wafike kuonana naye Januari 3, mwakani atakapokuwa Songea kwa mapumziko mafupi ya mwisho wa mwaka.

No comments: