Sunday, December 3, 2017

RC RUVUMA AWATAKA MAOFISA UGANI KUWA KARIBU NA WAKULIMA

Na Dustan Ndunguru,    
Songea.

MKUU wa mkoa wa Ruvuma Christine Mndeme amewataka maofisa  ugani na wataalam wa masuala ya kilimo mkoani humo, kuhakikisha kwamba wanasimamia kwa ukaribu maandalizi ya uzalishaji mazao mbalimbali, katika msimu wa kilimo mwaka 2017/2018 ili wakulima waweze kuzalisha mazao mengi na yenye ubora ambao utawafanya wapate bei nzuri sokoni.

Mndeme alitoa agizo hilo juzi alipokuwa akifungua kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa, kilichofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea mjini hapa.

Alisema kuwa msimu wa mvua kwa mwaka 2017/18 umeanza ambapo wakulima wanapaswa kwenda mashambani ili waweze kupata mafanikio katika kazi wanayofanya ya uzalishaji wa mazao mbalimbali.


Alisisitiza kuwa ni muhimu kwa wataalamu wa kilimo kuwatembelea mara kwa mara wakulima hao na kuwapa maelekezo ya kitaalamu namna ya kuzingatia kanuni bora za kilimo.

“Mvua hivi sasa zimeanza kunyesha, kuashiria kazi ya kilimo kuanza hivyo jukumu la maofisa ugani ni kihakikisha wanawafuata wakulima vijijini na kuwapa elimu ya namna bora ya uzalishaji wa mazao yao ili waweze kuzalisha kwa tija”, alisema.

Mkuu huyo wa mkoa alifafanua kuwa kuanzia msimu huu wa kilimo Serikali haitatumia mfumo wa pembejeo za ruzuku kama ilivyozoeleka katika kipindi cha miaka ya nyuma badala yake wakulima watanunua mbolea kwa bei elekezi itakayotolewa na Wizara ya kilimo.

Alibainisha kuwa lengo la utaratibu huo wa kutumia bei elekezi itakayotolewa ni kuweza kuwafanya wakulima waweze kupata mbolea za kupandia na kukuzia mazao yao shambani.

Vilevile aliongeza kuwa mfumo huo utawezesha wakulima wengi mkoani Ruvuma kuzalisha mazao mengi kama vile mahindi na kwamba aliwaagiza Wakuu wa wilaya na Wakurugenzi wa mamlaka za Serikali ya mitaa katika mkoa huo, kusimamia kikamilifu zoezi hilo mara Serikali itakapotoa maelekezo husika.

Mkoa huo  ni moja kati ya mikoa inayozalisha mazao mengi ya chakula na biashara hapa nchini ikiwemo mahindi ambapo katika msimu wa 2016/2017 ulivuna jumla ya tani  milioni 1,232,776  za mazao ya chakula aina ya wanga ambapo mahitaji halisi ya chakula ni tani  338,889 na kuufanya mkoa kuwa na ziada ya chakula tani 893,887.

Aliwataka wakulima kuzitumia vizuri mvua zinazoendelea kunyesha kwa kuzalisha mazao kwa wingi na kwamba wahakikisha wanazingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa kilimo kwenye maeneo yao badala ya kulima bila kuzingatia utaalamu hali ambayo husababisha wavune mazao kidogo yasiyo na ubora unaotakiwa kwenye masoko.

No comments: