Wednesday, December 27, 2017

KITUO CHA MABASI YA ABIRIA MADABA WAOMBA ZIONGEZWE CHANGARAWE KATIKA MAENEO AMBAYO MAGARI YANASIMAMA

Baadhi ya wachuuzi wa ndizi na biashara nyingine wakiuza bidhaa zao kwa abiria wa gari linalofanya safari zake kati ya Njombe na Songea katika kituo cha mabasi Madaba halmashauri ya wilaya ya Madaba Mkoani Ruvuma.



Na Muhidin Amri,      
Madaba.

KITENDO kilichofanywa cha kukarabati kituo cha Mabasi ya abiria Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mkoani Ruvuma, kimepongezwa huku baadhi ya abiria na wamiliki wa magari yanayobeba abiria hao wakiuomba uongozi wa halmashauri hiyo, kuongeza changarawe katika maeneo ambayo magari yanasimama katika kituo hicho.

Ombi hilo lilitolewa juzi kwa nyakati tofauti wakati abiria hao na watumiaji wengine wa kituo hicho walipokuwa wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari.

Walisema kuwa kazi iliyofanywa ya kukarabati miundombinu ya kituo hicho ni nzuri, lakini wanaomba katika maeneo ambayo magari yanasimama ziongezwe changarawe ili kuondoa hali ya utelezi ambayo hutokea hasa kipindi hiki cha masika.


Madereva wa magari ya abiria walipongeza hatua iliyochukuliwa na uongozi wa halmashauri hiyo walisema kazi iliyofanywa hapo ni nzuri, ambapo Erick Malecela ambaye ni dereva wa basi la abiria linalofanya safari zake kati ya mkoa jirani wa Njombe na Songea kupitia Madaba alisema, ukarabati huo umesaidia kushawishi madereva wengi kuingia na kutoka kwa ajili ya kushusha na kupakia abiria.

“Bado tatizo ni utelezi kwa baadhi ya maeneo kwani pindi mvua zinaponyesha tunapata tabu tunaiomba halmashauri kuangalia uwezekano wa kumwaga changarawe, badala ya kutumia udongo ambao sio rafiki sana ya maji hasa katika kipindi hiki ambacho mvua zimeanza kunyesha katika maeneo mengi”, walisema.

Pia Kituo hicho cha magari ya abiria ndicho ambacho kinategemewa kuwa ndiyo chanzo kikuu kimojawapo cha kuingiza mapato ndani ya halmashauri hiyo.

Andrew Msigwa ambaye ni mkusanyaji wa ushuru katika kituo hicho mbali na kuishukuru halmashauri kwa kazi ya ukarabati huo, ameliomba Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani kuhakikisha linachukua hatua kwa madereva wa mabasi ya abiria ambao wanakaidi kuingia ndani ya kituo wakati wa kushusha na kupakia abiria.

Alisema kuwa wapo baadhi ya madereva wasumbusu ambao hawataki kuingia kituoni hapo, jambo ambalo linasababisha halmashauri kukosa mapato yake ikiwemo fedha ambazo zingeweza kusaidia marekebisho mengine madogo madogo.

Mweka hazina wa halmashauri ya wilaya ya Madaba, Emmanuel Abraham alibainisha kuwa mpango uliopo wa halmashauri hiyo katika bajeti yake ya mwaka 2018/2019 ni kuhakikisha kwamba inaweka tabaka la lami katika kituo hicho, na kukamilisha ujenzi wa miundombinu yote muhimu inayohitajika ili watumiaji wa kituo hicho waweze kupata huduma zote za msingi ikiwemo kukamilisha ujenzi wa vibanda vya biashara vinavyozunguka kituo hicho.

No comments: