Sunday, December 31, 2017

NYAMAIGOLO AWAPA SOMO WAPIGA KURA UCHAGUZI MDOGO SONGEA



Na Dustan Ndunguru,       
Songea.

KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka kata ya Butobela, Wilayani Geita Mkoa wa Geita, Robert Nyamaigolo amewataka wapiga kura katika uchaguzi mdogo unaotarajia kufanyika Januari 13 mwaka huu katika jimbo la Songea mjini Mkoani Ruvuma, kuhakikisha kwamba wanamchagua mgombea wa Chama hicho ili aweze kutekeleza ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015 kwa vitendo.

Pia amewaasa watendaji, viongozi na wanaCCM kuainisha maeneo ambayo wapinzani walishinda katika uchaguzi wa Serikali za mtaa uliofanyika mwaka 2014 na kuyapangia mkakati kabambe utakaopelekea kuyarejesha mikononi mwa chama mwaka 2019.

Nyamaigolo alisema hayo juzi wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa kampeni ya uchaguzi mdogo wa Ubunge uliofanyika viwanja vya Majengo mjini hapa.


Alisema kuwa tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya awamu ya tano kasi ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi imekuwa kubwa jambo ambalo wananchi wengi wanaendelea kujenga imani na chama chao.

“Nawasihi wananchi wa Songea mjini waendelee kukiamini Chama cha mapinduzi na Serikali yake iliyopo madarakani kwani imekuwa ikiahidi na kutekeleza, hivyo mchagueni Ndumbaro ili aendeleze pale ambapo mtangulizi wake aliishia”, alisema Nyamaigolo.

Kada huyo kutoka Mkoani Geita alieleza pia baada ya kufanyika kwa uchaguzi huo kinachotakiwa ni kwa watendaji, viongozi na wanachama kupanga mikakati ambayo itakivusha chama katika uchaguzi wa Serikali za mitaa ujao ambapo wenyeviti wa vijiji, vitongoji na mitaa watachaguliwa.

Nyamaigolo alisema jambo la kwanza ni vyema yakaainishwa vizuri vijiji, mitaa na vitongoji ambavyo vinashikiliwa na wapinzani ambapo baada ya hapo yaorodheshwe yale ambayo yalisababisha CCM kushindwa kwenye maeneo hayo na kuyafanyia kazi kwa umakini mkubwa na kwa wakati ili uchaguzi huo unaokuja yote yarejeshwe mikononi mwa chama kinachotawala na sio vinginevyo.

Aliongeza kwa kuwataka wanaCCM kuandaa wagombea wenye sifa na ambao wanakubalika kwa wananchi na kwamba mabadiliko yaliyofanyika ndani ya chama hususan nyakati za chaguzi nayo yazingatiwe kwa ustawi wa chama tawala na kwa upande wa wale ambao bado wataendelea kufanya kazi kwa mazoea wawajibishwe ili iweze kuwa fundisho kwa wengine.

No comments: