Thursday, December 7, 2017

WAFANYABIASHARA WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA YA KUFUNGUKA KWA MIPAKA

Na Dustan Ndunguru,
Songea.

NAIBU Waziri wa kilimo Dokta Mary Mwanjelwa amewataka wakulima na wafanyabiashara  mkoani Ruvuma, kuchangamkia fursa ya kufunguka kwa mipaka kwa ajili ya kusafirisha mazao yao hususan mahindi ndani na nje ya nchi kwa kuzingatia kanuni na sheria zilizowekwa na Serikali.

Dokta Mary alisema hayo hivi karibuni wakati alipokuwa akizungumza na baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika, wakulima na maofisa ugani katika viwanja vya kituo cha ununuzi wa mahindi (NFRA) Kanda ya Songea mkoani humo.

Alisema kuwa Serikali katika kuwajali wakulima wake imeamua kufungua mipaka na kutoa fursa kwa wananchi wake wakiwemo wakulima, wafanyabiashara na kwa mtu mmoja mmoja kwa lengo la kuwawezesha kwenda kuuza mahindi yao nchi yeyote yenye uhitaji wa chakula.

Kadhalika aliwaomba wakulima hao kujiunga kwenye vikundi vya ushirika ili waweze kupata mikopo kwa urahisi kutoka kwenye taasisi za fedha, kuongeza thamani ya mazao yao ili waweze kupambana na walanguzi wanaopita kuwalaghai wakulima kwa kununua mazao yao kwa bei ndogo.

Waziri huyo amepiga pia marufuku  kuuzwa kwa mbolea rejareja na ya kupima  katika mitaa mbalimbali kwa madai kuwa  asilimia kubwa  inachakachuliwa na kuwasababishia wakulima kupungua kwa kiwango cha uzalishaji wa mahindi na kwamba ametoa onyo kwa yeyote atakayekaidi agizo hilo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Akiwa mkoani Ruvuma kwa ziara ya siku moja Naibu Waziri Mwanjelwa aliweza kutembelea na kukagua maghala ya kuhifadhia mahindi katika Kituo cha kununulia mahindi (NFRA) Kanda ya Songea pamoja na eneo la ujenzi wa maghala na vihenge na ujenzi wa kiwanda cha kuchakata mahindi cha OTC Lilambo kilichopo chini ya Halmashauri ya wilaya ya Songea.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano huo, mmoja wa wakulima hao Isiaka Mapunda alisema kuwa tatizo la ukosefu wa soko la kuuzia mahindi limesababisha baadhi yao kushindwa kumudu gharama za kununulia pembejeo za kilimo pamoja na kusomesha vijana wao.

Kwa upande wake John Komba mkulima kutoka kijiji cha Maposeni wilayani humo alimuomba Naibu Waziri huyo kuona umuhimu wa kuongeza tani za ununuzi wa mahindi  na kuiomba Serikali kupitia mfuko wa pembejeo wa kilimo kutoa mikopo ya pembejeo hizo kwa wakulima kwa wakati na riba nafuu.  

No comments: