Saturday, December 23, 2017

TUNDURU IDADI YA MAAMBUKIZI UKIMWI YAJA JUU



Na Muhidin Amri,       
Tunduru.

WATU 1,361 kati ya 54,698 sawa na asilimia 2.5 ambao wamefikiwa na huduma ya upimaji wa Virusi Vya Ukimwi (VVU) wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wamegundulika kuwa na maambukizi ya virusi hivyo katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi kufikia Oktoba mwaka huu.

Imeelezwa kuwa idadi hiyo ni kubwa ikilinganishwa na ile ya mwaka 2016 kwani watu waliopimwa walikuwa 24,459 na 756 waligundulika kuwa na maambukizi mapya ya VVU.

Mratibu wa kudhibiti ugonjwa wa Ukimwi wilayani humo, Dokta Vitalis Lusasi alisema hayo juzi alipokuwa akitoa taarifa ya hali ya maambukizi hayo katika wilaya hiyo.


Dokta Lusasi alisema kuwa kubainika kwa watu hao ni baada  ya idara ya afya kupitia kitengo chake cha kupamba na kuenea kwa maambukizi ya Virusi vya ukimwi, hospitali ya wilaya iliendesha zoezi la upimaji ambapo watu 54,698 ambao wanawake 34,262 na wanaume 20,436 walipimwa afya zao.

Alieleza kuwa idadi hiyo inaweza kuongezeka kwani matarajio ya upimaji kwa mwaka 2018 ni kuwafikia wateja 71,253 wilayani humo.

Aidha Dokta Lusasi alieleza kuwa huduma hiyo inatolea katika vituo 12 tu vya halmashauri ya wilaya ya Tunduru, ambapo hadi kufikia mwezi Desemba 2016 toka huduma hiyo ilipoanzishwa jumla ya wateja wapatao 7,513 walikuwa wamesajiliwa kwenye kitengo cha kutibu na matunzo ya watu wanaoishi na VVU.

Pia alibainisha kuwa wateja  5,506 wanawake 3,756 na wanaume 1,750 tayari walikuwa wanatumia dawa za kufubaza makali ya Virusi vya ukimwi.

Hadi kufikia mwezi Oktoba mwaka huu watu 8,493 wanawake 5,776 na wanaume 2,717 wanaoishi na VVU walipatiwa huduma ya dawa ambapo 6,665 wameanzishiwa dawa za kufubaza makali ya virusi hivyo.

Katika mkakati wa kupunguza maambukizi mapya Dokta Robert alisema, wamefanikiwa kupunguza kiwango cha maambukizi hayo toka asilimia 3.1 mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 2.5 mwaka 2017.

Dokta Robert aliongeza kuwa sambamba na huduma mbalimbali za kupambana na maambukizi hayo, matibabu ya magonjwa ya ngono yamekuwa yakitolewa kwa wananchi pale wanapogundulika kuwa na vimelea vya magonjwa ya ngono katika vituo husika vya kutolea huduma.

No comments: