Saturday, December 2, 2017

WANANCHI MBINGA WATAKIWA KULA MLO KAMILI ILI WAWEZE KUBORESHA AFYA ZAO

Mdhibiti wa ugonjwa wa Ukimwi wilaya ya Mbinga, Madebele Masumbuko akizungumza mambo mbalimbali na baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Kipololo iliyopo wilayani humo ambapo alikuwa akiwaelimisha pia juu ya athari za maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU). 
Na Mwandishi wetu,      
Mbinga.

WANANCHI wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wamesisitizwa kuzingatia kula mlo kamili ili kuweza kwenda sambamba na mambo mbalimbali ikiwemo kuwa na afya bora kwa faida ya maendeleo ya kizazi cha sasa na kijacho.

Vilevile imesisitizwa kuwa ulaji wa lishe bora unapaswa uendane na mchanganyiko wa vyakula ambavyo vina wanga, protini, mboga mboga, matunda na sukari.

Janeth Bandari ambaye ni Afisa lishe wa Halmashauri ya wilaya hiyo alisema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa kata ya Kipololo katika maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani.


“Tujitahidi kula mlo kamili kwa sababu mlo bora unajenga mwili na kumfanya mtu akue vizuri kimwili hata kiakili, binadamu unatakiwa upate lishe bora tokea pale unapozaliwa”, alisema.

Alifafanua kuwa binadamu akizingatia hilo anaweza kumjenga mtoto wake akue vizuri tokea anapokuwa tumboni mwa mama yake kabla ya kuzaliwa.

Pia alieleza kuwa wataalamu wa masuala ya afya wamekuwa mara kwa mara wakisisitiza hilo ili kuifanya jamii iendane na ulaji mzuri wa vyakula ambao unajenga mwili na kuweza kuepukana na magonjwa mbalimbali.

Pamoja na mambo mengine kwa nyakati tofauti wananchi wa kata ya Kipololo waliunga mkono na kueleza kuwa watazingatia hilo, kwani wao wamekuwa wakizalisha vyakula vingi vya aina tofauti ambavyo vinafaa kwa matumizi ya binadamu katika kuujenga mwili.

No comments: