Thursday, December 21, 2017

TUNDURU KUWAPATIA MICHE BURE YA KOROSHO WAKULIMA WAKE



Na Muhidin Amri,    
Tunduru.

HALMASHAURI ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma kwa kushirikiana na bodi ya korosho nchini, imeotesha miche bora ya zao la korosho 638,000 kwa ajili ya kuwapatia miche hiyo bure wakulima wake wanaozalisha zao hilo katika maeneo mbalimbali wilayani humo.

Afisa kilimo wa halmashauri hiyo, Chiza Malando alisema miche hiyo imezalishwa kupitia vikundi vya wakulima ambavyo vilipatiwa elimu juu ya uzalishaji huo na mwitikio wake katika utekelezaji wa jambo hilo umekuwa mzuri.

Lengo la kufanya hivyo ni kuweza kuongeza uzalishaji wa zao hilo ambalo ni tegemeo kubwa kwa kukuza uchumi wa wananchi wa wilaya hiyo.


Malando alisema, mpango huo ulianza tangu mwaka 2008 kupitia sekta ya  uendelezaji wa kilimo nchini, hata hivyo bado kulikuwa na mwamko mdogo ambapo kufikia mwaka 2016 waliweza kuzalisha miche 295,000 na mkakati wa halmashauri hiyo ulikuwa ni kuzalisha miche 658,000 katika ekari 21,000 kwa wakulima hao wa Tunduru.

Kwa mujibu Afisa kilimo huyo alibainisha kuwa tangu kuanza kwa mkakati huo mwitikio wa wakulima umekuwa mkubwa ambapo katika kutekeleza hilo miche 295,000 iliyozalishwa mwaka juzi ilionekana ni michache baada ya mahitaji ya wakulima kuwa makubwa.

Vilevile Malando alionesha kufurahishwa na uzalishaji wa korosho hizo kwa msimu uliopita ambapo wakulima wilayani humo waliweza kuzalisha tani 14,700 za zao hilo kiasi ambacho hakijawahi kufikiwa.

Alisema malengo ya halmashauri ni kuhakikisha kwamba wakulima wote wanawafikia ili waweze kuendelea kuboresha uzalishaji na kufikia kiwango bora zaidi cha uzalishaji ambapo wakulima wameanza kuondoa shambani mikorosho ya zamani na kupanda miche ya kisasa.

Aliwashauri wakulima wa korosho wilayani Tunduru kutumia vyema fedha wanazopata kwa ajili ya kufanya shughuli za maendeleo kwa kujenga nyumba bora, kusomesha watoto na kujiepusha na anasa ili  waweze kuondokana na umaskini katika familia zao.

Pia amewataka kutumia fedha hizo kwa kubuni miradi mingine ya kiuchumi kama vile ufugaji wa ng’ombe, kuku na mbuzi ambao watasaidia pia kujiongezea kipato  chao katika familia.

No comments: