Saturday, December 23, 2017

KUTOPATIKANA UMEME WA UHAKIKA KIKWAZO CHA MAENDELEO TUNDURU

Juma Homera, Mkuu wa wilaya ya Tunduru.


Na Mwandishi wetu,    
Tunduru.

BAADHI ya wakazi wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma wameipongeza Serikali ya awamu ya tano kwa hatua  ya kumaliza ujenzi wa barabara ya kutoka Namtumbo hadi Tunduru mkoani humo kwa kiwango cha lami.

Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti na mwandishi wetu Alli Mrope, Kassim Kassim na Rashid Uledi walisema kuwa kukamilika kwa barabara hiyo ni hatua moja mbele ya kuharakisha maendeleo ya wananchi wa wilaya hiyo.

Mrope alisema kuwa mbali na kuishukuru Serikali kwa ujenzi huo ameiomba pia kuendelea na mikakati ya kutekeleza miradi mingine ya maendeleo ambayo itasaidia kuharakikisha kukua kwa uchumi.


Alisema kuwa wilaya ya Tunduru ni kati ya wilaya ambazo zina  rasilimali nyingi hapa nchini, hata hivyo bado haijaweza kutumika vyema kutokana na kuchelewa kukamilika kwa miundombinu ya barabara na nishati ya umeme ambayo ni muhimu katika suala la kukua kwa uchumi.

Vilevile ameitaka Serikali kuangalia maeneo mengine ikiwemo huduma ya nishati ya umeme ambayo ni tatizo kubwa kwa wilaya hiyo kwa sababu itachelewesha mpango wa Serikali wa uanzishwaji wa viwanda.

Kassim alisema kuwa kukamilika kwa barabara ya lami kutoka Namtumbo Tunduru hadi Mang’aka mkoa jirani wa Mtwara ni jambo la faraja ambalo wananchi wa Tunduru wataendelea kuishukuru Serikali yao kwa kuwa muda mrefu barabara hiyo ilikuwa kikwazo kikubwa katika kupambana na umaskini.

Naye Mkuu wa wilaya ya Tunduru Juma Homera alisema Serikali imedhamiria kwa dhati kumaliza changamoto zote ikiwemo suala la umeme kwani tayari imeshaanza kusambaza nishati hiyo kwa baadhi ya vijiji kupitia mradi wa umeme vijijini REA.

Homera alisema tayari baadhi ya vijiji katika jimbo la Tunduru kusini vimeshapata umeme na kwamba REA imejipanga kuhakikisha kuwa vijiji vyote vya wilaya hiyo vinapata umeme haraka iwezekanavyo na kuwataka wananchi kuwa watulivu wakati huu ambao utekelezaji wake unafanyika.

No comments: