Wednesday, December 27, 2017

WATUMISHI WA UMMA HAPA NCHINI KITANZINI


Na Mwandishi wetu,

SERIKALI kupitia Sekretarieti yake ya Maadili hapa nchini, imewataka viongozi wote wa umma kujaza fomu ya tamko la maandishi ambalo linaorodhesha Mali au Rasilimali wanazomiliki, kabla ya kufikia Desemba 31 mwaka huu.

Rasilimali hizo ni zile zinazojumuisha mali za mke na mume pamoja na watoto wao ambao wamezidi umri kuanzia miaka 18 kuwasilisha kwa Kamishna wa maadili, ambapo kwenye tamko hilo litajumuisha mali na rasilimali za kiongozi husika.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 132 ya 1977 Sekretarieti hiyo ya maadili ya viongozi wa umma ni idara inayojitegemea chini ya Ofisi ya Rais, ambayo ilianzishwa kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma namba 13 ya mwaka 1995.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo, Kamishna wa maadili Jaji mstaafu Harold Nsekela alisema kuwa Sekretarieti hiyo inatoa wito kwa viongozi wa umma ambao hadi sasa bado hawajapata fomu, wapitie kwenye tovuti ya www.ethicssecretariat.go.tz ambapo huko ndipo zinapopatikana fomu za tamko hilo la rasilimali na madeni.

Alisema kuwa baada ya kujaza fomu hizo kiongozi atatakiwa kuziwasilisha katika Ofisi za Sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma Dar es salaam au katika Ofisi kanda ya kati Dodoma, kanda ya ziwa Mwanza na kanda ya nyanda za juu kusini iliyoko mjini Mbeya.

Vilevile viongozi wamekumbushwa kwamba ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 15 (C) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kiongozi kushindwa kutoa tamko bila sababu ya msingi.

Kwa upande wake Afisa sheria mkuu wa Sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma, Filotheus Manuca alisema kuwa katika kipindi cha mwaka jana hapakuwa na kiongozi yeyote ambae alifikishwa kwenye baraza la maadili na kusema kazi kubwa ya Sekretarieti hiyo ni kuhakikisha kwamba kila kiongozi wa umma anakuwa mwadilifu.

No comments: