Sunday, November 4, 2012

FARU YAMLIZA MAPUNDA RUVUMA


Na Dustan Ndunguru,
Songea.

CHAMA cha mpira wa miguu mkoani Ruvuma(FARU) kimepata viongozi wapya watakaoongoza chama hicho, kwa kipindi cha miaka minne ijayo.

Uchaguzi wa kuwachagua viongozi hao ulifanyika kwenye ukumbi wa Walimu SACCOS Songea mjini, ambapo mwenyekiti anayemaliza muda wake Joseph Mapunda alishindwa kutetea nafasi yake baada ya kubwagwa chini na Golden Sanga.

Akitangaza matokeo mwenyekiti wa kamati huru ya uchaguzi wa chama cha mpira wa miguu mkoani Ruvuma, ambaye pia ni katibu tawala wa wilaya ya Songea Joseph Kapinga alimtangaza Golden Sanga kuwa mwenyekiti kwa kupata kura 17 sawa na asilimia 53.13 dhidi ya  Joseph Mapunda aliyepata kura 15 sawa na asilimia 46.88.

Kapinga alimtangaza Dk. Zubery Kivo kuwa makamu mwenyekiti baada ya kupata kura 24 ambapo nafasi ya katibu mkuu ilinyakuliwa na Ahmad Challe baada ya kupata kura 17.

Katika nafasi ya katibu mkuu msaidizi ilichukuliwa na Ajabu Chitete aliyepata kura 14 na kwamba Deograsias Liganga alishinda nafasi ya mweka hazina baada ya kupata kura 29.

Nafasi ya mjumbe wa mkutano mkuu TFF ilinyakuliwa na Humphray Milanzi baada ya kupata kura 24 ambapo wajumbe wa kamati tendaji ni Emmanuel Komba aliyepata kura 24 na Kelvin Haule aliyepata kura 25 ambapo nafasi hiyo ilipaswa kuwa na wajumbe watatu lakini walioomba kugombea walikuwa wawili.

Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi nafasi ya uenyekiti, Sanga aliwataka viongozi wa wilaya na mkoa kwa ujumla kujenga ushirikiano katika kukuza kiwango cha soka mkoani Ruvuma, na kwamba atahakikisha anaimarisha mshikamano miongoni mwao.

No comments: