Tuesday, November 6, 2012

MADIWANI TUNDURU WATAKIWA KUACHA MALUMBANO



Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, wakimsikiliza mkuu wa wilaya hiyo Chande Nalicho (hayupo pichani) wakati wa kikao cha baraza la madiwani hao kilichofanyika mjini humo hivi karibuni.






Na Dustan Ndunguru,
Tunduru.

MADIWANI na watumishi katika halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kufanya kazi kwa ushirikiano  na kuachana na tabia ya kuendekeza malumbano yasiyo na tija kwa wilaya hiyo na kwa taifa kwa ujumla.

Mkuu wa wilaya hiyo Bw. Chande Nalicho alisema hayo kufuatia kuwepo kwa tofauti za kiutendaji katika halmashauri hiyo, zilizosababisha kuwepo kwa makundi baina  ya watumishi na  watumishi na baadhi ya madiwani hivyo kusababisha miradi ya maendeleo, kutokamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

Bw. Nalicho aliyasema hayo alipokuwa akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika mjini hapa, ambapo  aliwaagiza madiwani  hao kusimamia kwa umakini miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao, badala ya kusubiri taarifa za wataalamu ambao wakati mwingine wamekuwa sio waaminifu.

Alisema ili malengo ya serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo yaweze kufikiwa kama ilivyokusudiwa, madiwani na watendaji wanapaswa kuwa kitu kimoja na kwamba kuendekeza migogoro hakuwezi kuleta tija.

“Serikali imedhamiria kuwaletea watanzania maendeleo ya kweli na ndio maana ilikuja na kauli mbiu ya maisha bora kwa kila mtanzania, lakini kauli  mbiu hiyo imekutana na kikwazo cha watu wachache wanaokwamisha kwa maslahi yao binafsi”, alisema.

Aliwataka watumishi na madiwani ambao hawaelewani kumaliza tofauti zao kupitia vikao halali na kwamba ili wananchi wajenge imani na serikali miradi yote iliyobuniwa inapaswa kukamilika kwa wakati uliopangwa na kuanza kuwanufaisha wananchi hao.

Mkuu huyo wa wilaya ya Tunduru alisema  madiwani hawana budi kuacha kufika mara kwa mara katika ofisi zao za halmahauri bila ya kuwa na sababu za msingi, kwani kitendo hicho ndicho chanzo cha kuzalisha majungu na fitina kati yao na wataalamu.


No comments: