Saturday, November 10, 2012

WATEJA WA AIRTEL MONEY MBINGA WATAPELIWA


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

BENKI ya NMB tawi la Mbinga mkoa wa Ruvuma imesitisha huduma ya kuuliza salio, kununua na kutoa salio kwa njia ya simu kwa mtandao wa (AIRTEL MONEY) kupitia benki hiyo kwa baadhi ya wateja wake, ambao wametoa malalamiko, kwa kile kinachodaiwa kwamba mfumo huo umeingiliwa na matapeli ambao wanaiba fedha za wateja waliojiunga nao, kupitia akaunti zao ambazo wamezifungua katika benki hiyo.

Utafiti uliofanywa na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti umebaini kuwa, wateja walioibiwa fedha zao na ambao wamelalamika kutapeliwa kupitia mfumo huo, ni baadhi ya wafanyakazi wa halmashauri ya wilaya hiyo na wananchi wa kawaida.

Mwandishi wa habari hizi ameshuhudia hata mawakala wa mtandao wa airtel waliopo Mbinga mjini, wakisumbuliwa na wateja wao wakidai kwamba kuna watu kuanzia Alhamisi ya tarehe 25 Oktoba mkwaka huu mpaka sasa, walikuwa wakipigiwa simu na watu wanaojitambulisha kutoka makao makuu ya mtandao huo, kwamba wanatakiwa watoe baadhi ya taarifa za usajili wa laini zao za simu kwa kile walichoambiwa kwamba majina yao yamechaguliwa kwa ajili ya kuyashindanisha kwenye promosheni(michezo ya bahati nasibu) na baadaye wakishinda waweze kupata zawadi.

Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake, mmoja kati ya waathirika wa tukio hilo(ambaye ni mteja wa airtel) alisema yeye alipopigiwa simu hiyo aliambiwa kama ifuatavyo;

Namnukuu:
“Kwanza nilipigiwa simu na mtu ambaye alijitambulisha jina ambalo kwa sasa silikumbuki akisema, unaongea na makao makuu ya airtel, jioni hii tunafanya promosheni nyingine kama zile zilizopita kipindi cha nyuma katika mkoa wako”,

“Mshindi wa kwanza atapata milioni 30, wa pili 20 na watatu milioni 10, wewe ni mmoja kati ya watano walioteuliwa lakini watakaoshindanishwa katika promosheni hii ni majina matatu tu kati ya hayo matano”,

“Hivyo tunaomba ututajie kwanza huduma unazozitumia katika mtandao wa airtel, majina yako matatu, namba yako ya simu, mwaka uliozaliwa, mkoa uliopo, mtaa unaoishi na akaunti namba ya benki”.

Anasema baada ya kutaja vitu hivyo na maswali mengine mengi ambayo alikuwa akiulizwa, baada ya kumaliza maongezi tu na “tapeli huyo” aliyempigia, utakuta simu inakatwa mawasiliano na laini haifanyi kazi tena.

Anaeleza kwamba baada ya siku moja kupita alipokwenda benki alikuta salio lake limehamishwa, ndipo alipotoa taarifa kwa uongozi husika wa benki na kuchukua maamuzi ya kujaza fomu maalum kwa ajili ya tatizo lake kufanyiwa kazi.

Wateja ambao walijiunga na huduma hiyo ya mtandao wa airtel ambao baadhi yao wamefanyiwa hujuma kama hiyo, wamesitisha huduma ya airtel money katika benki ya NMB kupitia tawi la Mbinga, ambao taarifa zao zimeripotiwa katika benki hiyo na kujaza fomu maalum kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

Hivi sasa tunayo majina ya watu watano ambao wamejaza fomu hizo(majina na namba zao za simu tunayo) baada ya kufanyiwa hujuma hizo.

Kwa mujibu wa chanzo cha uhakika kutoka NMB kimedai kuwa tatizo hilo limekuwa likijitokeza maeneo mengi na wao sio mara yao ya kwanza kulisikia au kuletewa malalamiko kama haya, huku ikidaiwa kuwa linafanywa na wafanyakazi wa airtel ambao sio waaminifu.

“Wengine ambao wana namba zetu za simu hapa ofisini waliwahi kutupigia na kutuomba tuzuie akaunti zao baada ya kupigiwa simu na watu wanaodaiwa ni wa kutoka makao makuu ya airtel, sisi tukazuia akaunti zisifanye kazi kwa muda ili wasiweze kuibiwa,

“Lakini kwa wale waliochelewa, ndio kama hivi wameibiwa na tunawashauri hata kama kuna watu wanapigiwa simu za mtindo huu wazipuuze, wasiendelee kuongea nazo na kutoa taarifa za huduma zao za fedha za mtandao wa simu”, kilisema chanzo hicho.

Mwandishi wa habari hizi alipofanya mahojiano na Meneja wa mawasiliano wa airtel makao makuu Dar es Salaam, aliyejitambulisha kwa jina la Jackson Mbando(0786670120) alisema kampuni ya airtel hivi sasa haiendeshi mashindano ya promosheni.

Alisema utoaji na uwekaji wa pesa kwenye akaunti za wateja wa mtandao wa kampuni hiyo, endapo kuna tokea matatizo kama haya ni uzembe unaofanywa na wateja katika kutoa taarifa zao ikiwemo “Password”, hivyo wateja wanatakiwa kuwa makini kutotoa taarifa hizo ili wasiibiwe fedha zao.

Alisema kwa wale waliofanyiwa hivyo waende kuripoti kituo cha polisi, “Kitu kama hiki hakikuwa na sababu ya kuendelea kukijadili ni vyema nashauri waende polisi na taratibu za kisheria ziweze kuendelea”, alisema Bw. Mbando.

Pamoja na majibu hayo bado mwandishi wetu aliendelea kufanya mawasiliano kwa njia ya simu na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa kampuni ya airtel makao makuu Dar es salaam, naye alijitambulisha cheo hicho na jina lake, Beatrice Singano(0784670277) ambapo alipoulizwa juu ya hujuma hizo walizofanyiwa wateja wake hapa Mbinga, mkoani Ruvuma alisema,

“Sisi kampuni yetu haina taarifa juu ya tukio hili, na vilevile hatuendeshi promosheni, nasema sina taarifa ndio kwanza nimeipata kutoka kwako”, alisema.

Kadhalika aliongeza kuwa endapo taarifa hiyo itawafikia rasmi ofisini kwao, “Tupo tayari kutoa ushirikiano wa aina yoyote katika hili, mara tupatapo taarifa kamili, hivi sasa kwa kweli hatuna taarifa kamili juu ya tukio hili”, alisisitiza.


No comments: