Wednesday, November 7, 2012

TRA RUVUMA YAKUSANYA MILIONI 424.2


Na Mwandishi wetu,

MAMLAKA ya  mapato Tanzania(TRA) mkoani Ruvuma imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi milioni 424.2 kupitia mtandao wa utoaji leseni za udereva, katika kipindi cha mwaka 2011 hadi 2012.

Meneja wa mamlaka ya mapato wa mkoa huo Bw. Apili Mbaruku alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, kuhusiana na maadhimisho ya siku ya mlipa kodi ambapo kimkoa yanafanyika mjini Songea.

Bw. Mbaruku alisema kuwa kiasi hicho cha fedha  kilipatikana kutokana na utoaji wa leseni hizo, kwa watumiaji wa vyombo vya moto ikiwemo magari na Pikipiki.

 “Katika kipindi hicho leseni  mpya 8,500 zilitolewa na bado tunaendela kufanya mipango ya utoaji elimu kwa watu ambao hawajapata leseni hizo, ili hatimaye waweze kuhamasika kuzipata”, alisema.
 
Aidha meneja huyo alisema kwamba katika kipindi hicho mamlaka hiyo iliweza kuboresha mfumo wa ukusanyaji kodi kwa njia ya vitalu(Block management system) ambapo waliandikishwa walipa kodi 1,094.
 
Hata hivyo katika kipindi cha mwaka 2011/2012 mamlaka ya mapato Tanzania TRA mkoani Ruvuma, iliweza kukusanya shilingi bilioni 5.476 na kuvuka lengo walilopangiwa ambapo katika msimu wa mwaka 2012/2013 wamepangiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni saba.

 Pamoja na mafanikio hayo yaliyopatikana mamlaka hiyo pia inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo baadhi ya maeneo kushindwa kutumia mashine zinazotumika kutolea risiti na kutunza kumbukumbu, kutokana na ukosefu wa nishati ya umeme kwa wafanyabiashara waishio katika maeneo ambayo hayana miundombinu hiyo hususani vijijini.

No comments: