Thursday, November 1, 2012

WALALAMIKIA ZAHANATI KUTOKARABATIWA MUDA MREFU

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Bw. Shaibu Nnunduma.

Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.
 
WAKAZI wa kijiji cha Nyoni kata ya Nyoni Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamelalamikia kitendo cha Halmashauri ya wilaya hiyo kutokarabati zahanati ya kijiji hicho kwa miaka mingi iliyopita.  
 
Bw. Dominicus Kapinga mmoja kati ya mkazi wa kijiji hicho anasema hali ya zahanati hiyo sio nzuri kutokana na kutelekezwa kwa miaka mingi, na kwamba kijiji cha Nyoni ni moja kati ya vijiji maarufu wilayani humo ambavyo wakazi wake wameweza kupiga hatua mbalimbali za kimaendeleo, katika kilimo cha mazao ya chakula na biashara yaani kahawa na mahindi.
 
“Zahanati yetu ya kijiji imetelekezwa miaka mingi, ukizingatia kwamba ni kijiji chenye historia nzuri kutokana na hata Mwalimu Nyerere kutembelea hapa kuweka jiwe la msingi katika ofisi ya chama cha mapinduzi tawi la Nyoni”, anasema Kapinga.

 
Wakati huo huo nao wahudumu wa afya katika zahanati ya kijiji hicho na kituo cha afya cha Myangayanga wilayani humo, wamelalamikia nyumba wanazoishi kuwa ni chakavu zina hali mbaya jambo ambalo linahatarisha usalama wa maisha yao .
 
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti baada ya kutembelea katika maeneo hayo, walisema nyumba hizo zinahatarisha usalama wa maisha yao hasa kipindi hiki cha masika.
 
Nyumba mbili za waganga katika kituo cha Myangayanga zimejenga nyufa kubwa huku kuta zake zikiwa chakavu, na kwa zahanati ya Nyoni nyumba tatu wanazoishi waganga nazo ni chakavu hazijafanyiwa matengenezo siku nyingi.
 
Katika kijiji cha Nyoni mwandishi wa habari hizi ameshuhudia nyumba moja ya mganga kati ya hizo tatu, ikiwa imeezuliwa na upepo mkali ambao uliambatana na mvua kubwa, Januari 21 mwaka huu majira ya usiku, na kusababisha mganga aliyekuwa akiishi humo kuondoka na kwenda kupanga uraiani.
 
Wafanyakazi wanaoishi katika maeneo hayo wamekuwa wakipata shida kufuata maji umbali mrefu mtoni, kwa ajili ya matumizi ya kwenye vituo hivyo na matumizi yao binafsi ya nyumbani kutokana na maeneo hayo kutokuwa na miundombinu ya mabomba ya maji.
 
“Kwa kweli tunapata shida, tunaamka usiku wa manane kutafuta maji umbali mrefu ni vyema serikali isikilize kilo chetu na kumaliza kero hii mapema”, alisema mganga wa zahanati ya Nyoni Imelda Ndunguru.
 
Naye mganga mkuu wa kituo cha afya Myangayanga Bw. Athuman Songoro anasema kituo hicho kinakabiliwa na upungufu mkubwa wa madawa na vitendea kazi katika kitengo cha mama na mtoto ikiwemo hata akina mama wajawazito.
 
Bi. Esther Nyika ni mhudumu wa afya wa kituo hicho naye anasema nyumba wanazoishi zinavuja sana pale mvua zinaponyesha hivyo wanauomba uongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo kuangalia uwezekano wa kuzikarabati.
  
Nimeshuhudia nyumba mbili wanazoishi wafanyakazi hao wa kituo cha afya Nyoni, zikiwa kama gofu ambalo limetelekezwa miaka mingi.
 
 

No comments: