Tuesday, November 6, 2012

WANAFUNZI 2436 TUNDURU HAWAJARIPOTI KATIKA SHULE WALIZOPANGIWA KUENDELEA NA MASOMO, TATIZO LA UTORO NA MIMBA LIMEKUWA SUGU



Baadhi ya wazee wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, wakimsikiliza mkuu wa wilaya hiyo Bw. Chande Nalicho katika kijiji cha Chiwana wakati wa kilele cha wiki ya elimu ya watu wazima wilayani humo.







Na Dustan Ndunguru,
Tunduru.

WANAFUNZI 2436 waliopangwa kuanza kidato cha kwanza wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, baada ya kuhitimu darasa la saba mwaka jana hawajaripoti katika shule walizopangiwa kwenda kusoma, ambapo wanafunzi 1603 sawa na asilimia 35 ndio walioripoti shuleni kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utoro na mimba.

Akifungua kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri mjini hapa mwenyekiti wa halmashauri hiyo Bw. Faridu Hamis alisema wanaopaswa kulaumiwa hasa ni wazazi, ambapo pamoja na kuwepo kwa jitihada za makusudi za kuhamasisha watoto wanaofaulu mitihani yao ya darasa la saba waendelee na masomo bado jitihada hizo hazileti mafanikio.

Bw. Hamis alisema tatizo hilo sugu la wazazi kutowapeleka shule watoto wao ambao wamefaulu kuendelea na masomo ya sekondari, sasa limekuwa la kawaida kwa wazazi na walezi wa watoto hao na kwamba wakati umefika kuwachukulia hatua za kisheria ukizingatia kwamba huu si wakati wa kubembelezana katika masuala ya erlimu.


"Hebu waheshimiwa madiwani fikirieni hadi kufikia Julai mwaka huu kati ya watoto 2436 waliopangwa kuanza kidato cha kwanza, ni wanafunzi  1603 tu sawa na asilimia 35 ndio walioripoti mashuleni, jamani tunaenda wapi kwa kweli hili ni tatizo kubwa", alisema.

Alisema wilaya hiyo bado inakabiliwa na changamoto kubwa ya kuhamasisha wazazi wafahamu umuhimu wa elimu, ili watoto wao wanapofaulu kuwaendeleza kimasomo jambo ambalo litasaidia wapate uelewa na hatimaye kuwa na ujasiri wa kuendesha maisha yao kwa umakini mara watakapohitimu masomo yao.


Alieleza zaidi kuwa katika wanafunzi 883 ambao hawajaripoti wapo ambao  wamepata mimba tatizo ambalo ni sugu katika halmashauri hiyo, kwani wazazi wa watoto hao wamekuwa wakiwaficha waliofanya uhalifu huo na kukwamisha juhudi za serikali za kuhakikisha watoto wa kike, nao wanapata elimu sawa na ilivyo kwa watoto wa kiume.

Mwenyekiti huyo wa halmashauri alisema kuwa hivi sasa tayari msako mkali wa kuwatafuta wanafunzi ambao hawajaripoti katika shule walizopangiwa umeanza, hivyo wazazi wao ambao hawajawapeleka watoto wao shule watawafikisha mahakamani ili iwe fundisho kwa watu wengine ambao watafanya vitendo hivyo.

 



No comments: