Thursday, November 1, 2012

WAVUVI ZIWA NYASA WALIA NA SERIKALI




Upande wa kulia katibu wa kikundi cha wavuvi wa samaki Mbamba bay Bw. Agrey Ngonyani, akionyesha aina ya nyavu ambazo hutumika kuvulia samaki. Kushoto ni mvuvi wa samaki Bw. Simon Lwela, wakiwa karibu na ziwa Nyasa.





 
 
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

WANAFANYA kazi za uvuvi kwa kutumia vifaa duni, wavuvi hupoteza maisha yao, waiomba serikali kusikiliza kilio chao ili waweze kuondokana na matatizo wanayokabiliana nayo.
 
Hawa ni wananchi kutoka jamii ya wavuvi waishio katika mwambao mwa ziwa Nyasa wilaya ya Nyasa, mkoani Ruvuma ambao tegemeo lao la kukuza uchumi katika maisha yao ya kila siku ni shughuli za uvuvi.
 
Wamekuwa wakivua samaki wa aina mbalimbali na dagaa ambao huuza na wengine hutumika kwa kitoweo majumbani, pia wengine wamekuwa wakijishughulisha na kilimo cha zao la mhogo, mpunga, mbogamboga na matunda.
 
Lakini jitihada zao za uvuvi zinakwamishwa kutokana na kukosa zana za kisasa za uvuvi na hii inatokana na wananchi wengi kutokuwa na uwezo wa kumudu gharama za kununua maboti ya kisasa ambayo wangeweza kutumia kwa uvuvi.
 
Wameweza kuunda umoja wao wa wavuvi uitwao Samaki Business, uliopo katika mji mdogo wa Mbamba bay, na kusajiliwa mwaka 2009.
 
Umoja huu umekuwa ukivua samaki aina ya katoga, kambale na dagaa nyasa ambao huuzwa ndani  na nje ya mkoa wa Ruvuma .
 
Bw. Agrey Ngonyani ni Katibu wa umoja huo anasema samaki hao wanavua kwa mtindo wa kutega nyavu kuanzia nchi nne na kuendelea.
 
Anasema mikondo ya maji katika ziwa Nyasa imekuwa ya kasi hivyo wavuvi wanashindwa kuvua kutokana na kuwa na vifaa duni ambapo wamekuwa wakitumia mitumbwi jambo ambalo ni hatari kwa maisha yao .
 
“Wengi tumekuwa tukipoteza maisha, kwa mwaka hujitokeza vifo vya wavuvi kufa maji, visivyopungua watu watatu hadi wanne kutokana na uduni wa vifaa vyetu vya uvuvi,
 
“Uvuvi mwambao mwa ziwa hili ndio mama anaye tufanya tuishi, hata mzunguko wa fedha unatokana shughuli hizi za uvuvi”, anasema.
 
Bw. Ngonyani anasema wavuvi waliopo ni zaidi ya 100 katika kikundi chao hivyo wanaiomba serikali iwasaidie vifaa vya kisasa vya uvuvi kama vile maboti ya kisasa na sio kutumia mitumbwi kama ilivyo wanavyofanya sasa ambapo huwafanya washindwe kutimiza mahitaji yao ya kuvua samaki wengi.
 
Anabainisha kuwa kwa siku wamekuwa wakivua samaki tani 3 au zaidi na kuwahifadhi kwa mfumo bora unaotakiwa tayari kwa kusafirishwa kwenda kuuzwa.
 
Changamoto nyingine wanayokabiliana nayo ni kukosa meza za kuanikia ambapo kwa sasa hutumia matete kutengeneza meza za kuanikia, tekinolojia ambayo imekwisha pita na wakati.
 
“Tunaishukuru halmashauri yetu ya wilaya ya Mbinga, kutufikishia elimu sahihi ya uvuvi hivyo wavuvi wengi unaowaona hapa elimu hii imewafikia na wanavua kwa kufuata taratibu husika”, anasema Bw. Ngonyani.
 
Anaongeza kuwa suala la mikopo kwao imekuwa ni shida hivyo wanaziomba taasisi mbalimbali za kifedha kama vile mabenki kuwakopesha fedha ili waweze kuendesha umoja wao wa wavuvi uitwao Samaki business.
 
Bi. Bupe Kalikene ambaye anashughulika na uuzaji wa samaki na dagaa anasema, tatizo wanalokabiliana nalo ni kukosa soko la uhakika katika mauzo ya samaki na dagaa.
 
Anasema wamekuwa wakiuza kwa mtindo wa kuwasafirisha kwa marafiki zao na kupeleka Mbinga mjini au Songea na baada ya siku kadhaa hurejeshewa fedha mara baada ya mauzo kufanyika.
 
“Hakuna soko la uhakika, hakuna wafanyabiashara wanaokuja kununua hapa moja kwa moja bali tunafanya jitihada za kuuza sisi wenyewe”, anasema.
 
Baadhi ya wavuvi wengine suala la kuwa na vitendea kazi duni huwafanya kutumia nguvu kubwa katika shughuli hizo za uvuvi ili waweze kuuza na kupata fedha za kujikimu kimaisha.
 
Mvuvi Simon Lwena anasema samaki ni wengi katika ziwa Nyasa lakini wanashindwa kuwavua kwa wingi kutokana na kukosa zana borab za kisasa.
 
Bw. Lwena anasema hali hiyo inasababisha uhaba wa samaki ambapo wachache wanaopatikana bei yake huwa juu na kusababisha hali ya maisha yao kuwa magumu kwa wavuvi na wananchi wengine.
 
“Wakazi wa wilaya hii ya Nyasa hususani hapa Mbamba bay tusingekuwa na maisha magumu kama shughuli zetu za uvuvi zingekuwa zinafanywa kama maeneo mengine hapa nchini kwa kutumia vifaa vya kisasa”, anasema Lwena.
 
Anasema samaki hawa wa ziwa Nyasa ni wazuri na wanapendwa na watu wengi, kuna samaki wa aina nyingi lakini wanashangaa kwa nini serikali inashindwa kutumia ziwa hilo kama kivutio cha watalii na kufanya biashara kubwa ya samaki kama ilivyo katika ziwa Victoria.
 
Pamoja na mambo mengine anashauri kwa kuitaka serikali iwakopeshe mikopo ya fedha kupitia vikundi vyao vya uvuvi vilivyosajiliwa kisheria ili waweze kununua zana bora na hatimaye kuondokana na usumbufu wanaoupata sasa.
 
Ofisa uvuvi wa mji mdogo wa Mbamba bay aliyejitambulisha kwa jina moja la Mwasaga anasema, serikali inafanya utaratibu wa kuleta wataalamu wa kutengeneza maboti ya mbao ambayo yatafungwa injini kwa ajili ya kuwarahisishia wavuvi kufanya shughuli zao za uvuvi kwa ufasaha zaidi.
 
Bw. Mwasaga anaongeza kuwa juu ya suala la wavuvi kupewa mikopo wanapaswa kufanya jitihada zao za kuomba mikopo kupitia taasisi za kifedha ili waweze kuboresha shughuli zao na sio kuitegemea serikali peke yake.
 

No comments: