Wednesday, November 14, 2012

MWAFUTE: UTUNZAJI WA MAZINGIRA NI JUKUMU LETU SOTE

Ofisa misitu wa wilaya ya Mbinga, Bw. Vincent Mwafute.


















Na Mwandishi wetu,
Mbinga.

OFISA misitu wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Bw. Vicent Mwafute amewataka wananchi wilayani humo, kuacha tabia ya kukata na kuchoma moto misitu ovyo badala yake waitunze, ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Kauli ya ofisa huyo ilifuatia kutokana na kasi ya vitendo vya uchomaji moto misitu inayoendelea kufanyika wilayani humo.

Bw. Mwafute alisema idara yake imekuwa ikitoa elimu mara kwa mara kwa wananchi, juu ya utunzaji wa mazingira lakini watu wachache ndio wamekuwa kikwazo katika kufikia malengo.

Alisema ushirikiano wa dhati unapaswa kuwepo baina ya viongozi, maofisa misitu wa kata na wananchi kwa ujumla katika kukabiliana na suala hili linaloonekana kujitokeza kila mwaka hasa miezi ya Julai, Agosti, Septemba na Oktoba.


Alisema mwaka huu kasi ya uchomaji moto imekuwa ni kubwa ikilinganishwa na miaka mingine na kwamba uongozi husika umekwisha chukua hatua mbalimbali, vya kudhbiti vitendo hivyo ambapo tayari kuna baadhi ya wananchi wamekwishafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayowakabili ya uchomaji wa moto misitu.

"Sisi kama watendaji wa idara ya misitu tupo makini katika kukabiliana na watu wanaochoma misitu ovyo, mpaka sasa wapo ambao wamepelekwa mahakamani kuhusiana na suala hili lakini pia wapo ambao wanatafutwa kutokana na uharibifu huo”, alisema.

Pamoja na kushamiri kwa tabia ya uchomaji wa misitu halmashauri hiyo imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa wananchi wanaanzisha mashamba ya miti, na sasa wamekuwa wakipewa miche ya miti bure kupitia kwenye vitalu vya miche ya miti vilivyopo kijiji cha Kitanda, na hivi sasa mwamko umekuwa mkubwa kutoka kwa wananchi juu ya uchukuaji wa miti hiyo na kwenda kuipanda katika maeneo yao ikiwemo vyanzo vya maji.

Bw. Mwafute alisema zoezi la ugawaji wa miche hiyo bure ni endelevu hivyo amewataka wale ambao msimu wa mvua uliopita hawakufanikiwa kuchukua miche hiyo, mvua zitakapoanza kunyesha mwaka huu, waende na wakachukue ili waweze kupanda kwenye maeneo yaliyoharibiwa na mapya ikiwa ni kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na baadaye miti ikiwa mikubwa itawaingizia kipato.



No comments: