Saturday, November 3, 2012

MBINGA WAHOFIA KUTOROSHWA KWA MAKAA YA MAWE KATIKA MGODI WA NGAKA KATA YA RUANDA














   



                                  Mkaa wa mawe.

WAHOFIA UTOROSHWAJI WA MAKAA YA MAWE:

WANANCHI wa kijiji cha Liyombo kata ya Ruanda wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wameonyesha wasiwasi wao juu ya kudaiwa kutoroshwa kwa makaa ya mawe pamoja na ulipwaji wa  fidia watakazo pata kwa mali zao, baada ya kufahamika kuwa kijiji hicho kimejengwa juu ya mwamba wa makaa ya mawe ambayo yanatarajiwa kuanza kuchimbwa kabla ya mwisho wa mwaka huu iwapo taratibu za vibali kwa mwekezaji zitakamilika.

Baadhi ya wakazi  wa  kijiji hicho kilichopo katika kata ya Ruanda ambao ni Bw. Elia Hyera, John Mbepera na Joakimu Nchimbi wakizungumzia suala hilo wametoa wito kwa serikali kusimamia na kuhakikisha wanalipwa fidia pamoja na kuwa makini na kufuatilia sampuli za makaa hayo zinazopelekwa nje ya nchi kwa madai ya kwenda kufanya utafiti wa ubora wa makaa ya mawe kabla ya kuanza kuchimbwa.

Kampuni ya Tancoal Energy Limited (TANCOAL)  shirika la Taifa la maendeleo            ( NDC) pamoja  na Pacific Corporation ya Afrika Mashariki (PCAM) walianza utafiti wa kuchimba makaa ya mawe katika  kijiji cha Liyombo ambapo utafiti umebaini eneo hilo kuwa na mkaa wa kutosha  na wenye ubora. 

Utafiti huo ulianza  April mwaka 2008 kwa kuangalia wingi wa makaa ya mawe, unene wa mwamba na ubora wa makaa hayo na sasa yanachimbwa kwa wingi.

Utafiti huo ambao umefanyika katika kijiji hicho kwa miaka minne sasa umebaini kuwa kijiji cha Liyombo kipo juu ya mwamba bora wa makaa ya mawe ambapo TANCOAL   ina hisa ya asilimia 70. 

Mgodi huo umekuwa chanzo kikubwa cha utoaji wa makaa ya mawe hapa nchini na kusambaza kwa wahitaji wote wa nishati hiyo hapa nchini, vikiwemo viwanda na nje ya nchi na kwamba kitakuwa chanzo kikuu cha umeme kimataifa na msaada katika gridi  ya umeme ya taifa ambayo hivi  sasa umeme wake hautoshelezi na kusababisha makali ya umeme mgawo.

Mtaalamu wa miamba Bw. Alex Sostenes anasema makaa hayo ya mawe yamesambaa maeneo yote ya Ngaka na Liyombo pamoja na maeneo mengine  ya jirani  na kijiji cha Liyombo na kwamba mashine ya utafiti kwa utalaamu imetoboa shimo moja kijijini hapo ili kubaini wingi wa mkaa na ubora wake na kuwataka wanakijiji wasiwe na wasiwasi juu ya nyumba zao ama mali zao.

Hata hivyo mkurugenzi mkuu wa TANCOAL  Bw. Emmanuel Costantinides  amethibitisha kuwa  mkaa wa mawe wa kijiji cha Liyombo ni mkaa bora kutokana na majibu ya “ sampuri zilizopelekwa Afrika Kusini kwa uchunguzi kupitia Bandari ya Ndumbi Ziwa Nyasa.

“Kiasi cha tani 1000 zilisafirishwa kupelekewa nchini Afrika ya kusini kwa uchunguzi wa awali kwa madhumuni ya kujiridhisha ambapo matokeo yameonyesha dalili nzuri kuwa mkaa unaonyesha  ubora wake haufanani na mkaa wa mawe unaochimbwa katika nchi yeyote duniani, mkaa wa Mbinga  ni bora kuliko mikaa mingine yote duniani’’, alisisitiza.

Alisema tani 10,000  zinahitajika  kupelekwa nchini Afrika ya kusini  kama sampuri kutoka eneo la utafiti ili wanunuzi waweze kujiridhisha zaidi ingawa hali hiyo inaleta hofu kwa wakazi wa kijiji hicho, ambao wanashauri ni bora utafiti ungefanyika hapa hapa nchini ili kusifanyike hujuma ya kusafirisha maliasili kama hii, nje ya nchi kwa kisingizio cha utafiti huku watanzania wakibakia kuambulia mashimo kutokana na uharibifu wa mazingira.

Mgodi wa makaa ya mawe ya Liyombo na  Ngaka wilayani Mbinga umekadiriwa kuwa na zaidi ya tani 400 milioni za mkaa wa mawe. Kiasi hicho kwa mujibu wa wataalam, kinaweza kuchimbwa kwa kipindi cha zaidi ya miaka 100.

Sera Taifa ya madini ya mwaka 1997 inasisitiza juu ya sekta binafsi kuendeleza madini, na wakati huo huo Serikali ikiwa na jukumu la kuidhibiti, kuikuza, kuiwezesha  na kuiendelea. Sekta ya madini inachangia takribani asilimia 2.3 ya pato la Taifa, ambayo inakadiriwa kufikia asilimia 10 ifikapo 2025. (Posted by Jicho letu nuru ya jamii)



No comments: