Monday, November 26, 2012

WAFANYABIASHARA WAJERUHIWA NA MAJAMBAZI TUNDURU



Na Steven Augustino,
Tunduru.

WATU wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wamemvamia mfanyabiashara mmoja anayenunua mpunga na kujeruhiwa kwa silaha za jadi huku akikatwakatwa mapanga na kufanikiwa kuporwa fedha tasilimu.
Taarifa za tukio hilo zinadai kuwa maharamia hao walifanikiwa kupora shilingi milioni 4,500,000.

Licha ya kujeruhiwa mfanyabiashara huyo kadhalika wenzake aliokuwa nao ambao ni Nurudin Mshamu, maarufu kwa jina Chinga(30) aliyekuwa naye akipelekwa kununua mpunga katika kijiji cha Mpanji wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.



Mwingine aliyejeruhiwa katika tukio hilo alifahamika kwa jina la Mbela Mohamed(28) aliyekuwa dereva wa Pikipiki aina ya Sunlg, yenye namba za usajili T. 428 BNW ambayo alikuwa ameikodi majeruhi Mshamu kwa ajili ya kupelekwa katika shughuli za biashara hiyo ambayo walikuwa wakiifanya.
Taarifa za tukio hilo zinaeleza kuwa  uvamizi huo, ulitokea katika mteremko uliopo msitu wa kijiji cha Machemba ambapo wahalifu hao waliweka magogo njiani na kufanikisha kuwapora.
Akiongea kwa shida, majeruhi Mshamu alisema kuwa kabla ya kukumbwa na mkasa huo yeye na abiria wake walitia maafuta katika pikipiki hiyo katika kituo cha Matala Oil kilichopo mjini hapa, na kwenda kuchukua viroba vya mpunga kwa mtu aliyemtaja kwa jina moja la Kawanga.

Alisema wakiwa njiani katika kijiji cha Kidodoma tajiri yake alipigiwa simu na mtu aliyemtaja kwa jina moja la Bw. Chikambo
aliyedai kuwa ameandaliwa kuwapokea na kuwapeleka kwa mtu aliyedaiwa kuwa na mpunga huo.

Alisema baada ya tukio hilo yeye na mwenzake waliendelea na safari yao hadi katika kijiji cha Legezamwendo, ambapo walisimama kwa muda wa dakika 10 ndipo tajiri huyo walipomkuta akizungumza na watu wengine.
 
Bw. Mohamed aliendelea kueleza kuwa baada ya kuondoka kijijini hapo na kuendelea na safari yao, mara baada ya kuukuta mzigo walioufuata wakiwa njiani wakati wakirudi ghafla waliyakuta magogo njiani, na baada ya kupunguza mwendo ili kuyakwepa walijitokeza watu watatu na kuanza kuwashambulia kwa kuwapiga kwa marungu na mapanga hali iliyo wafanya waanguke na kupoteza fahamu katika eneo hilo ambalo magogo yaliwekwa.  

Alisema baada ya tukio hilo majambazi hao walichukua jukumu la kuwafunga kamba mikononi na miguuni na kuwaunganisha na magogo hayo, na baadaye kuchukua simu na fedha zao ambapo kati ya fedha hizo majeruhi Mohamed alinyang’anywa shilingi 57,000 na simu yake ya mkononi.
Akizungumzia tukio hilo Mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Tunduru ambako wamelazwa majeruhi hao, Dkt. Fredrick Weinand alisema kuwa hali zao ni mbaya zinahitaji uangalizi wa karibu kutoka kwa maafisa tabibu ili kuokoa maisha yao.
Dkt. Weinand aliendelea kufafanua kuwa katika tukio hilo majeruhi
Mshamu(Chinga) aliumizwa vibaya kichwani kutokana na kukatwa kichwani mara tatu na begani upande wa mkono wake wa kushoto, huku Mohamed akionekana kuteguliwa misuli ya kiuno na miguu na kumfanya  kushindwa hata kuinuka na kutembea.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma Bw. Deusdedit Nsemeki
amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo, na kuongeza kuwa polisi
wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na kuahidi kuwa sheria
itafuata mkondo wake, baada ya watuhumiwa hao kupatikana.

No comments: