Monday, November 26, 2012

HALMASHAURI YATENGA BAJETI YA SHILINGI MILIONI 40 KWA MIRADI YA KILIMO

Na Dustan Ndunguru,
Songea.
HALMASHAURI ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, imetenga kiasi cha shilingi milioni 40 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kilimo katika kipindi cha mwaka 2012 hadi 2013.

Mwenyekiti wa kamati ya uchumi ujenzi na mazingira Bw. Teofanes Mlelwa, alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu, juu ya utekelezaji wa miradi ya DADPS katika kipindi hicho.

Bw. Mlelwa ambaye pia ni diwani wa kata ya Wino Songea vijijini,  alivitaja vijiji vitakavyonufaika na fedha za mradi huo wa maendeleo ni Mpandangindo, Matimira ambavyo vitalima zao la alizeti, Wino na Lilondo na Liganga vitajikita katika kilimo cha zao la kahawa, ambapo vijiji vya Muhukuru Nakawale na Ngadinda vyenyewe vitashughulika na kilimo cha zao la korosho na kwamba kijiji cha Magingo kitajihusisha na kilimo cha zao la Tangawizi ifikapo June 2013.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Bw. Rajabu Mtiula, alisema mkakati uliowekwa ni kuhakikisha kuwa pindi fedha hizo zinapopatikana, kipaumbele cha kwanza kitolewe kwa vijiji vinavyojishughulisha na kilimo cha zao la korosho.

Naye diwani wa kata ya Muhukuru Agatha Gama, aliiomba halmashauri hiyo kutoa elimu ya upuliziaji wa dawa mikorosho kwa wananchi wa kata hiyo, ukizingatia kwamba miti mingi ya zao hilo iliyokwisha pandwa imegeuka kuwa kichaka na makazi ya Ngedele kutokana na wananchi hao kushindwa kuihudumia kunakosababishwa na ukosefu wa elimu.

Kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Songea Wenisaria Swai, alisema kuwa pindi halmashauri yake itakapopata fedha, atahakikisha elimu ya utunzaji wa zao la korosho inatolewa kwa wananchi katika vijiji husika.

Alisema endapo zao hilo litatunzwa kikamilifu linaweza kuwa chanzo kimoja wapo cha kuiongezea halmashauri hiyo mapato na kuinua uchumi wa wananchi wa wilaya ya Songea, hivyo jukumu kubwa lililopo ni kwa wataalamu wa kilimo kuhakikisha wanatoa elimu ya namna ya utunzaji wa zao hilo kwa wakulima kila mara.

Aliwataka wakulima nao kwa upande wao kujiunga pamoja na kuanzisha mashamba darasa, ili iwe rahisi kufikiwa na maofisa ugani ambao kimsingi ni wachache na mara baada ya kupata elimu wajitahidi kuzingatia misingi watakayopewa, ili hatimaye waweze kuzalisha mazao bora yatakayowapa bei nzuri sokoni.

                  


No comments: