Friday, November 9, 2012

USAMBAZAJI WA PEMBEJEO ZA KILIMO MBINGA UZINGATIE TARATIBU ZILIZOWEKWA





Mahindi yakiwa yameoteshwa shambani kwa kufuata kanuni bora za kilimo.













Na Dustan Ndunguru,
Mbinga.

WAKULIMA 34,752 wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma watanufaika na pembejeo za ruzuku katika msimu wa kilimo wa mwaka 2012/2013 ikiwa ni pungufu ikilinganishwa na wakulima 46,517 waliopata pembejeo hizo msimu uliopita.

Akiongea na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake ofisa kilimo na ushirika wa wilaya hiyo Bw. Yonas Nyoni alisema msimu wa mwaka 2011 hadi 2012 jumla ya vocha 139,551 zilipokelewa ikilinganishwa na msimu huu wa mwaka 2012 hadi 2013 ambapo jumla ya vocha 104,256 zinatarajiwa kupokelewa.

Bw. Nyoni alisema kuwa katika msimu huu wa kilimo mahitaji halisi ya mbolea ni tani 28,652.60 na mahitaji ya mbegu ni tani 398 na kwamba alizitaja mbegu hizo kuwa ni za mahindi aina ya chotara tani 350, mahindi 0PV tani 45 na mpunga tani 3.


Alisema mbolea aina ya urea zinahitajika tani 9,550.90,minjingu tani 9,550.90 DAP tani 4,775.40 na S/A tani 4,775.40 na kwamba tayari makampuni yaliyopewa kazi ya kusambaza pembejeo hizo kwa wakulima yamekwisha anza kazi ya kuleta wilayani humo.

Alieleza kuwa idara ya kilimo wilayani humo ilikwishawaelekeza wakulima juu ya umuhimu wa kujiwekea akiba ya kutosha, ili kwa mkulima ambaye hatapata pembejeo za ruzuku aweze kununua pembejeo kutoka kwenye maduka ya wafanyabiashara binafsi kwa ajili ya kuboresha mazao yaliyomo   shambani.

Kadhalika kwa wale watakaobahatika kupata pembejeo za ruzuku wazitumie kwa malengo yaliyokusudiwa.

Vilevile aliyataka makampuni kumi ambayo yamepewa kazi ya kusambaza pembejeo hizo kwa wakulima, kuhakikisha kwamba yanatekeleza majukumu yao ipasavyo na kwa wakati ili wakulima waweze kuzitumia na hivyo kuwawezesha wazalishe mazao mengi na yaliyo bora.

Alisema kuwa serikali mwaka huu imeamua kuanzisha mfumo mpya wa usambazaji wa mbolea ambapo makampuni ndiyo yaliyopewa dhamana ya kusambaza kwa wakulima, na kwamba makampuni hayo nayo yataandaa mawakala wao ambao watazifikisha pembejeo hizo kwa mkulima husika.                            

Pia ofisa kilimo huyo aliwataka maofisa ugani wilayani Mbinga kuhakikisha katika ngazi za kata na vijiji, kuhakikisha wanatoa elimu kwa wakulima ili hatimaye waweze kuzalisha kwa kutumia utaalamu na kwamba wakulima nao, kwa upande wao wazingatie maelekezo yanayotolewa na wataalamu kupitia mashamba darasa yaliyopo.

No comments: