Wednesday, November 14, 2012

WANAJESHI KUTUMWA BARAGOI

Polisi aliyejeruhiwa Baragoi














Rais Mwai Kibaki wa Kenya ameidhinisha mpango wa kuwatuma wanajeshi, katika eneo la Samburu Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo kufuatia kuuawa kwa maafisa wa polisi na wezi wa mifugo ambao waliwavizia.

Takriban maafisa 42 wa polisi waliuawa, katika tukio ambalo limetajwa kuwa baya zaidi katika historia ya Kenya.

Baada ya kuongoza kikao cha dharura la baraza la usalama, rais Kibaki amesema, wanajeshi hao wametumwa katika eneo hilo kuwasaka wezi hao wa mifugo na kujaribu kurejesha mifugo hiyo iliyoibwa pamoja na kuwapokonya silaha.

Ripoti zinasema mamia ya watu wametoroka kutoka eneo hilo wakihofia mashambulio ya kulipiza kisasi.


Maafisa hao wa polisi walishambuliwa siku ya Jumamosi iliyopita karibu na mji wa Baragoi wakati walipokuwa njiani kuwafuata wezi hao wa mifugo.

Habari zinasema waliofanya mashambulio hayo walitumia silaha nzito kama vile mabomu ya kudungua magari na makombora ya gruneti.

Kiongozi mmoja wa kidini ambaye hakutaka jina lake litajwe, ameiambia BBC kuwa wakaazi wa eneo hilo wanahofu kuwa maafisa wa usalama wanaweza kuwanyanyasa wakati wa operesheni hiyo ya kuwasaka walioendesha mashambulio dhidi ya maafisa wa polisi.

Eneo hilo hukaliwa na watu wa jamii ya Samburu na Turkana ambao mara kwa mara huibiana mifugo na kugombea maeneo ya malisho ya mifugo.(BBC News)

.

No comments: